Usafi na Kinywa na utunzaji wa meno
WEKA TANGAZO
WEKA TANGAZO
Assalamu aleykum wasikiliziaji
wapenzi na karibuni katika kipindi kingine cha Ijuwe Afya yako. Kipindi
ambacho hujadili masuala mbalimbali yanayohusu afya na tiba kwa lengo la
kupata maarifa ya kuzitunza vyema afya na siha zetu. Katika kipindi
cheti cha leo tutazungumzia usafi wa kinywa na umuhumu wake na jinsi
utunzaji wa sehemu hiyo ya mwili unavyoathiri afya ya mtu kwa ujumla.
Karibuni.
&&&&&&&&
Afya ya kinywa ina umuhimu mkubwa zaidi
ya unavyoweza kufikiria na kwa ujumla inaweza kutoa ufahamu kuhusiana na
jinsi afya yako ya mwili ilivyo. Kuelezewa uhusiano uliopo kati ya afya
ya kinywa na afya ya mwili mzima kunasaidia kufahamu umuhimu wa kutunza
kinywa na hasa meno na fizi. Kama zilizo sehemu nyingine za mwili,
kinywa nacho kimejaa bakteria ambao wengi wao hawana madhara. Kwa
kawaida mfumo wa kulinda mwili na utunzaji mzuri wa kinywa kama vile
kupiga mswaki na kutumia uzi kuondoa uchafu katika meno kunaweza
kudhibiti bakteria walioko kinywani wabakie katika hali ya kawaida na
kutodhuru kinywa. Lakini bila kutunza vyema kinywa, bakteria hao
wanaweza kusababisha maambukizo na kusababisha meno kuoza na maradhi ya
fizi.
Afya ya kinywa inajumuisha siha na namna
ya utunzaji wa sehemu zote za mdomo hasa meno na fizi. Mbali na kinywa
kutuwezesha ipasavyo kula, kuzungumza na hata kuwa na muonekano mzuri wa
uso, meno na fizi zinapaswa zisiwe zimedhurika na kuwa na matatizo kama
vile meno kuoza, magonjwa ya fizi, kung'oka meno na mdomo kunuka. Kuoza
meno na meno kuwa na matundu ni matatizo ya kinywa yanayoshuhudiwa sana
miongoni mwa watu. Sababu zinazoweza kuzuia matatizo hayo ya meno ni
kudumisha usafi wa kinywa, kupata fluoride ya kutosha na kutokula kwa
wingi vyakula vinavyoweza kudhuru meno na kusababisha matundu.
Afya ya meno na kinywa kwa ujumla
inahusiana na afya ya mwili mzima kwa njia tofauti. Kwanza kabisa uwezo
wa kutafuna chakula na kukimeza ni muhimu ili mwili uweze kupata
virutubisho muhimu vya kujenga mwili. Halikahalika kuwa na kinywa chenye
matatizo kunaweza kuathiri namna mtu anavyozungumza na hata kujiamini
kwake. Matatizo ya meno yanaweza kumsababishia mtu gharama kubwa ya
matibabu na ukarabati wa meno.
Sababu zinazoweza kuathiri afya ya kinywa
Uimara wa meno na fizi unatofautiana
kati ya mtu na mtu, na umbo la taya, mdomo, meno na hata kiasi cha mate.
Hayo yote ni mambo muhimu yanayoweza kuainisha kwa nini baadhi ya watu
meno yao yanaoza zaidi kuliko wengine. Baadhi ya meno yanaweza kuwa na
vishimo na nyufa zinazoweza kuruhusu bakteri na tindikali kupenya kwa
urahisi na baadhi ya wakati umbo la taya huweza kuzuia meno
yasisafishike vizuri na kuondoa vyema uchafu kinywani. Kiwango na namna
mate yalivyo pia huweza kuathiri uozaji wa meno. Kwa mfano matundu na
nyufa huwa haziko sana katika meno ya mbele ambako kuna mate mengi
ikilinganishwa na meno ya nyuma. Bakteria wote walioko kinywani wanaweza
kubadilisha wanga kuwa tindikali lakini aina ya streptococci na
Lactobacili wana uwezo mkubwa wa kutengeneza tindikali. Kuwepo kinywani
vijidudu vya aina hii huongeza uwezekano wa meno kuoza. Baadhi ya watu
wana kiasi kikubwa cha bakteria wanaosababisha meno kuoza kuliko watu
wengine na hii ni kutokana na kuzembea katika kutunza na kuimarishwa
usafi wa kinywa.
Wataalamu wanatwambia kuwa, usafi wa
kinywa na matumizi ya dawa za meno zenye fluoride hupunguza kasi ya meno
kuoza. Usafi wa meno ni pamoja na kupiga mswaki kila siku kwa kutumia
dawa za meno zenye flouride, kutumia uzi wa meno kusafisha eneo lililo
kati ya meno, kuchokonea meno kwa kijiti ili kundoa mabaki ya chakula na
kufanyiwa uchunguzi wa meno mara kwa mara. Flouride huzuia kupungua
madini katika molekuli za meno, kuongeza madini hayo kwenye meno na
kuimarisha meno ili yasiathiriwe na tindikali. Matumizi ya fluoride kwa
kiwango kinachotakiwa huzuia na kudhibiti matundu kwenye meno. Flouride
inaweza kupatikana kutoka katika maji ya kunywa na baadhi ya vinywaji
vilivyoongezwa mada hiyo. Pia mada hiyo hutiwa katika dawa za mswaki,
geli na dawa za kusafishia kinywa. Katika baadhi ya nchi mada ya
fluoride huongezwa hata katika chumvi na maziwa. Kiwango cha flouride
katika maji ya kunywa na vyakula kinapaswa kuzingatiwa kwa mujibu wa
mahitaji ya mwili. Suala hili ni muhimu kwa watoto walio na umri wa
chini ya miaka 6 ambao meno yao bado yanakua. Kutumiwa sana au kwa
kiwango kikubwa mada hiyo husababisha matatizo katika enamel au mfupa wa
jino hali inayojulikana kinaalamu kama kama fluorosis.
Vyakula na athari yake katika kuoza meno
Ijapokuwa katika nchi nyingi kuoza meno
kumekuwa kukiambatanishwa na matumizi ya fluoride na utunzaji wa kinywa,
aina ya vyakula anavyokula mtu pia ni jambo muhimu linalochangia meno
kuoza. Jinsi chakula chenyewe kilivyo kwa mfano kama kinanata na
kung'ang'ania kwenye meno pia husababisha meno kuoza. Vyakula
vinavyong'ang'ania kwenye meno kama vile bisikuti na crips huongeza
uwezekano wa kuoza meno kwani hubakia juu ya meno kwa muda mrefu zaidi
kuliko vyakula vingine. Pia vyakula vyenye sukari zinazoyeyuka kwa
haraka husafishwa kwa wepesi kinywani na mate, na kila vyakula vyenye
wanga vinavyokaa muda mrefu kinywani na kuzunguka meno, ndivyo bakteria
wanavyopata fursa zaidi ya kutengeneza tindikali na kuondoa madini
katika meno. Kila tunapokula vyakula vyenye wanga, bakteria walioko
kwenye kinywa huanza kutengeneza asidi suala linalopelekea meno kuoza.
Mwenendo huu huendelea hadi baada ya dakika 10 hadi 20 baada ya kula au
kunywa. Katika kipindi tusichokula au kunywa mate huzimua tindikali na
kusaidia kurejesha madini katika meno. Iwapo vyakula au vinywaji
vitaliwa mara kwa mara na kinywa kisipate muda wa kurejesha madini
kwenye meno, hapo ndipo meno huanza kuoza. Kwa ajili hiyo tunashauriwa
kutokula na kunywa wakati wote na pia kupunguza kula vyakula vyenye
wanga na sukari kwa uchache tusile vyakula hivyo zaidi ya mara 6 kwa
siku. Pia tunashauriwa kuhakikisha kuwa tunapiga mswaki meno kwa kutumia
dawa za meno zenye fluoride, kwa uchache mara mbili kwa siku.
Mmomonyoko wa meno
Mmomonyoko wa meno ni kuharibika tishu
ngumu ya juu ya meno kutokana na acidi bila kuathiriwa na bakteria
wanaosababisha meno kuoza. Kuna vyakula na vinywaji vingi vyenye
tindikali katika lishe zetu na kuna uwezekano suala hilo likatuathiri.
Kwa mfano kupendelea sana kula vyakula au kunywa vinywaji vyenye
tindikali husababisha mmomonyoko wa meno. Tatizo hilo lisiposhughulikiwa
huweza kuathiri ufanisi wa kinywa na hutofautiana baina ya watu. Ili
kuepukana na tatizo hilo tunashauriwa kujiepusha kupenda sana kunywa
vinywaji au kula vyakula vyenye acidi na kupiga mswaki kwa uchache mara
mbili kwa siku kwa kutumia dawa ya mswaki yenye fluoride. Pia
tunashauriwa kutopiga mswaki mara tu baada ya kunywa au kula chakula
chenye acidi kwani kufanya hivyo huweza kuyafanya meno yaharibike
kutokana na kusugua meno wakati tindikali ikiwemo kinywani. Pia ni bora
tujizoeshe kutafuna chingamu au ubani mara tu baada ya kula vyakula
vyenye acidi ili kufanya mate yatengenezwe ambayo husaidia kuondoa acidi
mdomoni.
&&&&&&&
Naam wasikilizaji wapenzi, mada hii
kuhusu usafi wa kinywa na meno ndio kwanza imeanza, na tutaendelea
kuijadili pia katika kipindi kijacho. Hadi wakati huo, daima tuimarishe
afya zetu!
0 maoni: