Dawa za nywele zinazosababisha uvimbe wa kizazi.
WEKA TANGAZO
WEKA TANGAZO
Na Hudugu Ng'amilo
Dawa za
kulainisha nywele (relaxer) zimekuwa zinapendwa na wanawake wengi wa
Afrika kwa kuwa zina uwezo wa kulainisha nywele na kumfanya apendeze na
awe wa kuvutia.
Hata
hivyo, wataalamu wa afya wanadai kuwa dawa hizo zinasababisha uvimbe
kwenye kizazi kutokana na kemikali za dawa hizo ambazo huingia mwilini
kupitia majeraha au ngozi wakati wa kupaka.
Daktari
wa Manispaa ya Ilala, Laurent Chipata alifanya utafiti na kubaini kuwa
dawa za nywele na vipodozi zina kemikali ambazo husababisha uzalishwaji
wa vichocheo kwa kiasi kikubwa na kusababisha uvimbe kwenye kizazi
uitwao fibroids au leimyoma.
"Kemikali
hizi hupenya kwenye ngozi na wakati mwingine hata kwa harufu tu,
husababisha kuzalishwa kwa wingi wa vichocheo aina ya estrogen ambavyo
huchangia kuota kwa uvimbe wa fibroids," anasema.
Dk
Chipata anasema kukua kwa uvimbe kwenye kizazi hutokea katika kipindi
ambacho mama yupo kwenye uzazi yaani kabla hajakoma hedhi.
Utafiti
wa Dk Chipata ulifanywa nchini na kujumuisha wanawake wa kada tofauti
tofauti wanaotumia dawa za nywele na wale wasiotumia na ukubwa wa tatizo
hili ulibainika.
"Zipo
kemikali tofauti tofauti zinazosababisha uvinbe kwenye kizazi, zipo za
kwenye dawa za kilimo kama DDT na za kwenye mafuta ya ngozi kama vile
mercury na hydroquionone," anasema.
Dk
Chipata anasema madhara yanayopatikana katika kemikali za vipodozi ni
makubwa siyo tu kwenye kizazi bali nyingine husababisha saratani au
kufeli kwa figo. Anatoa mfano wa kemikali ya zebaki (mercury).
"Dawa za
nywele zina madhara si lazima zipenye kwenye ngozi baada ya mtu kupata
jeraha la kuungua bali zinaweza kupenya zenyewe kwenye ngozi kutokana na
mfumo wa ngozi," anasema.
Anashauri
kuwa ni vyema watu wakasoma kipodozi kimetengenezwa kwa nini kabla ya
kukitumia na kuongeza kuwa ni salama zaidi kubaki na ngozi au nywele
halisi badala ya kujibadilisha.
Mamlaka
ya Chakula na Dawa (TFDA) imekataza vipodozi vyenye kemikali kama
biothionol, hexachlorophene, mercury, vinyl chloride, zirconium na
bidhaa zenye aerosol, chloroquionone, steroids, methylene na chloroform.
Utafiti
mwingine uliofanywa mwaka 2012 na Dk Lauren Wise na wenzake nchini
Marekani na kuchapishwa kwenye jarida la afya la nchini Marekani
ulibaini kuwa vipodozi vingi vina kemikali zenye vichocheo vya estrogen
ambavyo kwa kawaida huchochea kasi ya kuota kwa uvimbe kwenye kizazi cha
mwanamke na wakati mwingine kwenye mji wa mimba. Kitaalamu uvimbe au
vivimbe hivi hujulikana kama fibroids au myoma.Dk Wise anasema
aliwafanyia uchunguzi wanawake wanaotumia dawa za kulainisha nywele na
kuangali umri walioanza kutumia dawa hizo, mara ngapi, waliungua kiasi
gani na walikaa na dawa hizo kichwani kwa kipindi gani.
Aliwafuatilia
wanawake 23,580 wanaotumia dawa za kulainisha nywele na baada ya
kipindi fulani walipimwa. Kati yao, 7146 waligundulika kuwa na uvimbe
kwenye kizazi baada ya kupimwa kwa mionzi na wengine kufanyiwa upasuaji.
Kwa nini relaxer ni hatari kwa wanawake?
Dk Wise
anasema mchanganyiko ulio kenye dawa za nywele hasa zilizoandikwa "Lye
Relaxer" ni sodium hydroxide wakati makopo ya dawa yaliyoandikwa "No Lye
Relaxer" yana calcium hydroxide na guanidine carbonate.
Bidhaa za
kulainishwa nywele zilizoandikwa 'no lye relaxer' zinadaiwa kusababisha
majeraha kwa kiasi kidogo ukilinganisha na zile zilizoandikwa "Lye
Relaxer".
Uvimbe kwenye kizazi ni nini?
Ukuta wa
nyumba ya uzazi umejengwa kwa misuli ya tishu. Kwa kawaida uvimbe huu
huanza kidogo kidogo na hukua hadi kufikia ukubwa wa tikiti maji.
Fibroids kubwa huweza kukua na kutanua nyumba ya uzazi na kuwa sawa na
ujauzito wa miezi sita au saba.
Mwanamke huweza kuwa na uvimbe mmoja mkubwa au vivimbe vingi ndani ya kizazi.
Daktari
Bigwa wa magonjwa ya uzazi wa Kitengo cha Upasuaji cha Chuo Kikuu
Sayansi ya Tiba Muhimbili, Henry Mwakyoma anauelezea fibroids ni uvimbe
ambao upo katika umbile la misuli myembamba na laini linalokua siku hadi
siku.
"Sababu inayopewa kipaumbele zaidi ni wingi wa vichocheo vya estrogen ambavyo vipo katika miili ya wanawake," anasema.
Dk
Mwakyoma anafafanua kuwa, vichocheo hivi ndivyo hufanya kazi katika
mwili wa mwanamke na kumsababishia kupata siku zake za hedhi.
"Ndiyo
maana wengi wanaopata uvimbe huu, huwa ni wanawake walio katika umri
mkubwa au ambao tayari wamevunja ungo, kwani ndiyo ambao huzalisha
vichocheo vya estrogeni," anabainisha mtaalamu huyo."Dalili hutegemeana
na eneo ulipokaa uvimbe na ukubwa wake. Wengi hugundulika wakati wa
kujifungua au endapo mwanamke atapata uvimbe katikati ya kizazi, basi
huweza kutokwa damu kwa wingi," anasema.
Anaongeza: "Hata hivyo, asilimia 35 hadi 50 ya wanawake wanaougua maradhi haya huonyesha dalili wakati wa kujifungua,"
Dalili
nyingine ni mwanamke kutokwa damu zake za hedhi kwa wingi na kwa siku
nyingi. Damu za hedhi huweza kuwa nyingi au kidogo sana zikiambatana na
maumivu makali.
Anasema wakati mwingine mwanamke huweza kuhisi ana ujauzito kwani uvimbe huu huwa mkubwa na huchezacheza kana kwamba ni kiumbe.
"Nina
mifano hai, wapo wanawake waliowahi kuhisi wana ujauzito, wakakosa
kabisa siku zao za hedhi, wakaona dalili zote za mimba na kumbe walikuwa
na uvimbe wa fibroids," anasema.
Msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwanza anasema wamekuwa wakifanya ukaguzi mara kwa mara kuzuia uuzwaji wake.
Isitoshe
akasema: "Elimu inatolewa kwa wananchi pia ili kuwafahamisha kuhusu
madhara ya vipodozi hivyo kwa sababu wanunuzi wasipokuwepo basi hata
biashara haitakuwepo."
Pamoja na hayo, adhabu hutolewa ya kuwanyang'anya na kuwapeleka mahakamani wenye maduka makubwa wakiziuza.CHANZO MWANANCHI.
0 maoni: