Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo BBC. Onyesha machapisho yote

Mtoto wa Simba amlilia mamake

0 maoni
Simba huyo aliwaelekeza walinzi hadi katika mzoga wa mamake
Mtoto wa simba aliwaongoza askari wa kulinda wanyama kwenda ulipo mwili wa mama yake ambaye alikuwa ameuawa katika mbuga moja ya kuhifadhi wanyama nchini India, kitendo ambacho maafisa wa wanyama pori wanakilelezea kuwa si cha kawaida.
Askari wa wanyama pori ambaye alimwona mtoto wa Simba akijificha vichakani, alimfuata na kugundua mwili wa Simba aliyeuawa katika kilima jirani.
Mtoto huyo wa simba aliulinda mwili wa mama yake hadi pale mlinzi wa wanyama pori aliporudi na maafisa wa wanyama pori na polisi kuondoa mzoga huo.
Uchunguzi uliofanyiwa mwili wa simba huyo ulibainisha kuwa alikufa katika mapigano na wanyama wengine huenda aliuawa na kundi la nyati.
Naibu mhifadhi wa Misitu katika eneo la Gir, Anshuman Sharma, amesema tabia ya simba huyo mtoto ni nadra kutokea na ni cha aina yake, kitu ambacho hajawahi kushuhudia katika miaka yake mingi ya kufuatilia tabia za simba.
Gir katika jimbo la Gujarat ni mahali wanapopatikana kwa wingi simba wa Asia na kwa mujibu wa sense ya wanyama iliyofanyika mwaka 2010, kuna simba 411 katika mbuga hiyo.
"Jumamosi mchana, nilikuwa nafanya doria katika hifadhi ya Tulsi-Shyam nilipomwona mtoto wa simba akichificha katika vichaka,"mlinzi wa msitu Rana Mori ameiambia BBC.
''Watoto wa Simba huambatana na mama zao''
Watoto wadogo wa simba nadra kuwakuta peke yao , kwa ujumla wanafuatana na mama zao na Bwana Mori anasema alianza kumtafuta mama ya simba huyo mtoto.
"Nilimfuatilia mtoto wa simba ambaye aliniongoza hadi kwenye mwili wa mama yake uliokuwa umelala katika kilima kidogo. Simba huyo jike aliitwa Rupa [likiwa na maana ya Mzuri].Kwanza alionekana kama aliyelala usingizi, lakini wakati hatikisiki, nilimsukuma na fimbo yangu. Ndipo nilipogundua kwamba simba huyo jike alikuwa amekufa," amesema.
Wakati Bwana Mori aliporejea na kundi la maafisa kuondoa mzoga huo, walimkuta mtoto huyo wa simba akiwa amekaa kando ya mwili wa mama yake.
Simba huyo jike ambaye alikuwa na umri wa miaka kumi na moja , alivunjika mbavu na kupata majereha ya ndani na kufa kutokana na kuvuja damu nyingi.
Mtaalam wa Simba Yadvendra Dev Jhala wa taasisi ya Wanyama Pori ya India ameiambia BBC kuwa hajawahi kusikia tukio kama hilo linalomhusu mtoto wa simba.
''Simba na walinzi wao''
Lakini amesema katika eneo la Gir hakuna mgogoro kati ya simba na binadamu na "kwa ujumla Simba wanawafahamu vizuri walinzi wao binafisi ".
Bwana Sharma anasema wanafahamika kwa tabia yao ya maisha ya kijamii: "Si kama Mbwa, hawatoi kucha au kutikisa mikia, lakini wanawatambua walinzi wanaowaona kila siku.."
Maafisa wa wanayama pori wanasema kwa ujumla watoto wa simba ni wategemezi mno wa mama zao kwa ajili ya maisha yao hadi wanapofikia umri wa miaka miwili na nusu hadi mitatu.
Mtoto huyo wa simba mwenye umri wa miezi 15, kwa sasa yuko chini ya uangalizi wa maafisa wa misitu.
"Mama yake, Rupa, alionekana kuwa mpweke na aliwinda peke yake,Lakini kwa sasa simba huyo jike ametoweka, tunatarajia mtoto huyo wa simba atajiunga na kundi lingine, au simba mwingine jike huenda akaanza kumtunza," amesema Bwana Sharma.

Ni majonzi wazazi wakiandamana Nigeria

0 maoni
Wazazi waliandamana kuishinikiza serikali kuongeza kasi ya kuwatafuta watoto wao
Wazazi wa wasichana 230, waliotekwa nyara Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, wamefanya maandamano kuiomba serikali ya Nigeria kuongeza juhudi na kasi ya kuwatafuta watoto wao waliotekwa nyara na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Boko Haram.
Wasichana hao walikuwa wanafunzi katika mji wa Chibok na walitekwa nyara wakijiandaa kufanya mitihani yao zaidi ya wiki mbili zilizopita.
Mzazi mmoja ambaye hakutaka kutajwa , alisema kuwa wanashukuru wanigeria kwa kuwaunga mkono huku maandamano mengine yakifanyika kuwashinikiza maafisa wakuu.
‘‘Tunataka kuona juhudi zaidi,’’ alisema mama huyo
Kundi la wapiganaji la Boko Haram, halijasema chochote kuhusu madai kwamba wapiganaji wake ndio waliowateka nyara wasichana hao usiku wa tarehe 14 mwezi Aprili.
Wazazi walijawa na majonzi wakati wa maandamano wakisema serikali inajikokota
Kundi hilo ambalo linapinga elimu ya kimagharibi , limekuwa likifanya mashambulizi Kaskazini mwa Nigeria, na inakisiwa kuwa watu 1,500 wamepoteza maisha yao mikononi mwa kundi hilo mwaka huu pekee.
Mnamo siku ya Jumatano, mamia ya wanawake waliandamana wakiwa wamevalia nguo nyekundu licha ya mvua kubwa kunyesha na kutembea hadi majengo ya bunge mjini Abuja kuwasilisha ujumbe.
Wanailalamikia serikali kwa kusema haifanyi juhudi za kutosha kuwanusuru wasichana hao.
"Tunawashukuru wanawake waliotuunga mkono,'' alisema mama huyo akiongeza kuwa maandamano huenda yakashinikiza serikali kuongeza kasi ya kuwatafuta watoto wao.
Tunawaomba na wale walio huko nje kuja kutusaidia kwa sababu huu ni msiba mkubwa kwa wazazi wetu.
Alipokuwa anaongea, kilio na mayowe yaliweza kusikika kutoka kwa akina mama wengine waliokuwa wanaandamana.
Awali waziri wa mambo ya ndani wa Nigeria aliambia BBC kuwa alielewa hisia za wanawake hao, lakini serikali haiwezi kufichua inachofanya kujaribu kuwanusuru watoto hao.

Wapiganaji wavamia bunge Libya

0 maoni
Watu waliokuwa wamejihami walivamia majengo ya bunge nchini Libya Jumanne jioni na kulazimisha wabunge kusitisha shughuli ya kumteua waziri mkuu mpya.
Maafisa wanasema kuwa wabunge waliondoka bunge punde waliposikia milio ya risasi.
Hatua ya kupigia kura waziri mkuu mpya imetokana na kujizulu kwa aliyekuwa waziri mkuu Abdullah al-Thinni, aliyeondoka mamlakani mapema mwezi huu baada ya yeye pamoja na familia yake kulengwa na wapiganaji.
Libya imekuwa ikikumbwa na mgogoro tangu harakati za kumuondoa mamlakani hayati Muammar Gaddafi mwaka 2011.
Awali ripoti zilisema kuwa watu kadhaa walijeruhiwa katika mashambulizi siku ya Jumanne.
Haijulikani nani aliyehusika na shambulizi hilo.
Mwandishi wa BBC mjini Tripoli,Rana Jawad anasema kuwa bunge la Libya limewahi kuvamiwa na watu waliojihami katika kipindi cha mwaka mmoja unusu iliopita.
Wabunge wamekuwa wakitofautiana kuhusu kuteuliwa kwa waziri mkuu wakati shambulizi la Jumanne lilipotokea.
Tayari walikuwa wamefanya duru ya kwanza ya kura na kuwateua wagombea wawili kati ya saba.
Lakini duru ya pili ilipoanza ndipo watu hao waliposhambulia bunge na kulazimisha wabunge kuahirisha shughuli hiyo ambayo sasa itafanyika tarehe 4 mwezi Mei.

Watoto 9,000 walitumiwa vitani Sudan:K

0 maoni
Zaidi ya watoto 9,000 wamekuwa wakitumiwa kama wanajeshi katika vita vivayoendelea nchini Sudan Kusini.
Taarifa hii ni kwa mujibu wa mkuu wa haki za binadamu katika umoja wa Mataifa Navi Pillay.
Pande zote kwenye mgogoro huu , wanajeshi na waasi wamedaiwa kuwasajili watoto kupigana.
Bi Pillay amesema kuwa Sudan Kusini inakabiliwa na tisho la njaa , lakini viongozi wake hawaonekani kuliona hilo kama swala muhimu la kushughulikiwa.
Alikuwa anazungumza mwishoni mwa ziara yake nchini Sudan Kusini ambako mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe umewaacha mamiioni ya watu bila makao.
Vita vilizuka mwezi Disemba kati ya wanajeshi wa serikali wanaomtii Rais Salva Kiir na hasimu wake kiongozi wa waasi, Riek Machar ambaye anatuhumiwa kwa kuanzisha mgogoro huu kwa kuwa na njama ya kumuondoa mamlakani.
Riek Machar pia wakati mmoja alikuwa makamu wa Rais wa Salva Kiir.
Machar amekanusha madai hayo lakini amekuwa akiongoza waasi wanaopigana dhidi ya serikali.
Pande zote mbili zimekuwa kwenye meza ya mazungumzo kujaribu kusitisha vita lakini hakuna mabadiliko katika hali inayokumba nchi hiyo, Vita vingali vinaendelea.

Kikwazo kwa wanawake wanaovuta Shisha

0 maoni
Shisha
Je ni lazima mwanamke anayekwenda kujiburudisha katika kibanda cha kuvutia Shisha aambatane na mwanamume ambaye ni maharamu wake au jamaa wake ambaye hawezi kumuoa awe mlinzi wake?
Majadala huu umekuwa ukigonga vichwa kwenye mitandao ya kijamii nchini Saidi Arabia.
Mjadala ulianza baada ya picha ya mkahawa mmoja kuwekwa kwenye Twitter.
Mkahawa huo unawaruhusu tu wanawake walioambatana na mlinzi kuingia ndani na kuvuta Shisha.
Bila mlinzi wako basi huwezi kuruhusiwa kuingia kwenye kibanda hicho.
Shisha, ambayo pia inaitwa Hookah, huvutwa na wanaume sawa na wanawake katika nchi za kiarabu.
Ni mrija ulio kwenye kifaa kirefu hivi ambacho hutumiwa kuvuta Tumbaku ambayo imewekwa ladha ya matunda na huvutwa hasa na watu wanapojiburudisha.
Mjadala uliwaka moto kwenye mtandao wa Twitter baadhi wakisema: ''Shisha ni marufuku......wanawake hawaruhusiwi kuvuta ikiwa hawajaambatana na mlinzi.''
Hata hivyo mwanamke mmoja alijibu...''hilo halitushangazi kilichosalia ni kusema lazima pia tupewe ulinzi tukienda kuoga.''

Mlinzi na Shisha

''Msichana akivuta shisha hahitaji ulinzi,'' amesema mkereketwa mmoja
''Je itakuwa vipi ikiwa nitavuta shisha ikiwa huyo mlinzi wangu yuko chooni?'' alihoji mwanamke mwingine. Wanaume pia walijiingiza kwenye mjadala huo, wakisema kwa mzaha ....''Itakubidi unilipe dola hamsini ukitaka niwe mlinzi wako.''
Lakini kuna baadhi waliosema ni vyema....''uamuzi huu ni mzuri ili kupunguza athari za Shisha miongoni mwa wasichana wadogo. Kuna wasichana ambao huenda mikahawani kwa kujificha.''
Katika ukanda wa Gaza wanawake wamezuiwa kuvuta Sisha.
Mwanamke mmoja alisema ,'' msichana akitaka kuvuta Sisha hahitaji kufanya hivyo mbele ya mtu mwingine. Nadhani ni chuki tu dhidi ya wanawake na haja ya wanaume kutaka kuwatawala wanawake. Hiyo ndio chanzo cha sheria za kibaguzi kama hizo.''
Mfumo wa kuwalinda wanawake wanapotoka nje ya nyumba zao unajulikana kama Maharam na unazingatiwa sana nchini Saudi Arabia.
Mafumo huo unahitaji mwanamke kupata idhini kutoka kwa jamaa wake mwanamume ambaye hawezi kumuoa , mfanao kama kakake au mjombake ili aweze kusafiuri , kwenda kazini , kufanya harusi, au hata kupokea matibabu.
Wanaharakati wanapinga mfumo uu wakisema unawanyima wanawake haki zao.