Ndoa Na Sababu Za Kuchokana
WEKA TANGAZO
DINI
(...فاظفر بذات الدين تربت يداك...)
HALI YA KIJAMII NA KIUCHUMI
KIWANGO CHA ELIMU
KABILA
NDUGU WA KARIBU
HITIMISHO
Takriban katika maisha ya wanandoa walio wengi kama sio wote, ndoa zao
hupitia katika vipindi tofauti. Kama ulivyo umri wa Binadamu, ndoa
hupitia katika kipindi cha utoto, ujana na uzee, na kila kipindi kina
mambo yake na taratibu zake kama tulivyoona katika makala zilizopita
ambazo kama wanandoa watashindwa kuzifuata basi huenda ndoa hiyo
ikakumbwa na mtihani mkubwa, nao ni mtihani wa kuchokana.
Hivyo
basi, sababu kubwa ya wanandoa kuchokana, au kuzeeka kwa ndoa
kunasababishwa na mwanamke, pale ambapo atashindwa kutumia nafasi yake
na vipawa alivyopewa kuleta utulivu katika ndoa yao.
Leo
InshaAllaah tutahitimisha mfululizo wa makala haya kwa kugusia baadhi ya
nukta ambazo ni muhimu kwa wanandoa kuzizingatia kabla na hata baada ya
ndoa yao.
DINI
Kigezo Kikuu
cha kusimamisha ndoa ni Dini, na ndoa yoyote inapokuwa haikuzingatia
kigezo hiki basi ndoa hiyo inakuwa ina misukosuko isiyoisha, na si tu
inapelekea wanandoa kuchokana, bali inapelekea wanandoa kutengana na
kuchukiana. katika zama tulizonazo zama ambazo umagharibi umetawala
katika mila na desturi zetu, kigezo cha Dini kimepuuzwa na familia
nyingi za Kiislamu, na hata ainisho la neno ‘Dini’ limefahamika vibaya;
Dini inaonekana ni imani ya kuzaliwa nayo, na si matendo na utaratibu
wa maisha ya mtu. Na hii kupelekea mafunzo mengi ya Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutofahamika katika usahihi wake,
kwa mfano ile Hadiyth mashuhuri ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) iliyopokewa na Imaam Al-Bukhaariy inayohimiza
kumchagua mchumba mwenye Dini:
(...فاظفر بذات الدين تربت يداك...)
(mchague
mwenye dini utafanikiwa), mafundisho haya ya Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) yamekuwa yanatafsiriwa vibaya na wakati
mwingine hata na Mashaykh, kuwa mwenye Dini ni yule Muislamu, hata kama
haivai hijaab, haswali, fedhuli, lakini muda wa kuwa amezaliwa Muislamu
basi huyo ana Dini, ufahamu huu umewaingiza wanandoa wengi katika
mitihani.
Bali wakati mwingine, unamkuta msichana
amejihifadhi vizuri, anaswali lakini akhlaaq zake mbaya, msengenyaji,
mfitinishi, hapendi ndugu wa mume, mchoyo na imani ya kweli haijagusa
katika moyo wake, yeye huvaa Hijaab kama sehemu ya mila, na anaswali
Swalah tano kutokakana na makuzi yake na mashinikizo ya kijamii, lakini
hamna athari yoyote inayopatikana.
Hivyo basi, ni muhimu kwa
wanandoa wahakikishe kuwa ndoa yao inajengwa katika msingi mkuu na
imara, msingi wa Dini kwa maana yake sahihi.
HALI YA KIJAMII NA KIUCHUMI
Katika
ujenzi wa ndoa imara, kuna vigezo vingine ambavyo si muhimu lakini
havipaswi kupuuzwa, miongoni mwa vigezo hivyo ni kiwango cha wanandoa
kijamii na kiuchumi, hiki ni kigezo ambacho kinaweza kuonekana ni cha
kidunia zaidi, lakini uzoefu unaonyesha kuwa kimekuwa ni moja miongoni
mwa sababu zinazopelekea chokochoko katika familia na hatimae kuikwaza
ndoa yenyewe.
Inapotokea kwa mmoja miongoni mwa wanandoa hususan
mwamume akawa na hali duni kiuchumi kuliko ile ya mkewe (familia ya
mkewe) basi pamoja na mapenzi yanayowaunganisha, maisha yao yatakuwa na
tahadhari kubwa sana, na wakati wowote kinaweza kutokea kitu ambacho
hakikutarajiwa na kikazua mtafuruku.
Hivyo basi, ni vema wanandoa
wakaanza kujenga misingi imara ya ndoa yao kwa kujitahidi kuzingatia
kigezo hiki cha Kiuchumi na Kijamii.
KIWANGO CHA ELIMU
Aidha
ni muhimu kigezo hiki nacho kikazingatiwa katika ujenzi wa ndoa imara,
kwani wanandoa kama tulivyoona katika makala zilizotangulia, wanahitaji
kuwa na mazungumzo baina yao, mijadala tofauti tofauti na kubadilishana
mawazo katika maisha, inapokuwa elimu ya mwanamke ni kubwa kuliko ya
mwanamume, kwa mfano, mwanamke anapokuwa na shahada ya Chuo Kikuu, na
mwanaume ya Darasa la Saba, hapa panahitaji hekima na juhudi kubwa kwa
mwanamke kuweza kumuelimisha mumewe bila ya kumfanya ajihisi mjinga,
zoezi ambalo ni gumu, na uwezekano wa kushindwa ni mkubwa. Mwandishi wa
makala hii, ana ushahidi tosha wa ndoa zilizoharibika kutokana na kigezo
hiki. Nawe msomaji unaweza kufanya utafiti wako binafsi kuhusu hoja
hii.
KABILA
Uislamu
unayazingatia makabila kuwa ni sehemu ya watu kufahamiana, na si
vinginevyo, na umekaripia vikali ubaguzi wa aina zote zile ukiwemo
ubaguzi kwa misingi ya ukabila, utaifa, na rangi, na katika hili kuna
Aayah nyingi sana na Hadiyth nyingi za Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa
aalihi wa sallam).
Kwa upande mwingine, jamii zetu za Kiislamu
bado kwa kiwango kikubwa zinajenga mahusiano katika misingi ya ukaribu
wa kikabila na uzoefu wa pamoja, Uislamu haujakataza mtu kujinasibisha
na nasaba yake, kuipenda na kuitakia kheri, bali uislamu umekataza mtu
kujifakharisha kwa ukabila na kudharau makabila mengine.
Jamii
za Kiislamu pamoja na kuunganishwa na Qur-aan na Sunnah za Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lakini pia kila jamii
inaunganishwa na vionjo vyake, na urfu zake ambazo huenda zikawa tofauti
na jamii nyingine ya Kiislamu. Kwa mintarafu hiyo, ndoa inayowajumuisha
watu wa kabila moja, inakuwa ina uimara zaidi kuliko ndoa tofauti, na
inakuwa haina mashinikizo hasi kutoka katika jamii ukilinganisha na ile
nyingine.
NDUGU WA KARIBU
Uislamu
umeruhusu kwa baadhi ya ndugu wa karibu kuoana, mfano mtoto wa baba
mkubwa kwa baba mdogo, mama mkubwa kwa mama mdogo, mjomba kwa shangazi,
na ndoa hizi zimeenea sana katika baadhi ya jamii, na hata Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuozesha binti yake Faatwimah
(Radhiya Allaahu ‘anha) kwa mtoto wa ammy yake ambae ni 'Aliy Bin Abi
Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu), jambo la kushangaza ni kuwa baadhi ya
Waislamu hususan huku Afrika wamejiharamishia ndoa za aina hiyo, bila ya
dalili, jambo ambalo ni kwenda kinyume kabisa na mafundisho ya
Kiislamu.
Ndoa za ndugu wa karibu, zinaweza zikawa ni
sababu ya kuimarika kwa ndoa au sababu ya kudhoofika, lakini kwa uzoefu
wetu imeonekana kuwa ndoa za aina hii mara nyingi zinafikia katika hatua
ya uzee mapema zaidi, hii ni kutokana na kufahamiana kwa ndugu hawa
tangu utotoni, na kila mwanandoa kutotarajia jipya kutoka kwa mwenzake.
HITIMISHO
Ndoa
ndio msingi wa Familia, na familia ndio tofali la kwanza la kujenga
Jamii na hatimae kujenga Ummah, ndoa ni hatua muhimu sana anayopitia
bianadamu katika maisha yake, na ndio hatua inayoiathiri maisha ya mtu
na maisha ya kizazi chake baadae. Ni muhimu mtu kuwa makini sana na
hatua hii.
Kwa wale ambao tayari wameishaingia katika hatua hii,
basi ni muhimu kwao kuizatiti ndoa yao na mafundisho sahihi ya Uislamu
na kujaribu kurekebisha madhaifu yao kwa kuwa wawazi baina yao na
kupeana mawaidha kwa njia ya upole na hekima.
Maradhi ya
kuchokana katika maisha ya ndoa ni maradhi yalioenea kwa wanandoa wengi,
wapo wengine ambao hudhihirisha wazi hisia zao hizo kwa wenziwao, na
wengine ambao huwa wanajaribu kuficha hisia hizo.
Ni jukumu la
kila mwanandoa kuelewa ukweli huo, na kujaribu mara kwa mara kuleta
mabadiliko mema katika maisha yao, au kuikarabati ndoa kwa maana
nyepesi.
Mwisho
WEKA TANGAZO
0 maoni: