Mtoto wa Simba amlilia mamake
WEKA TANGAZO
WEKA TANGAZO
Mtoto wa simba aliwaongoza
askari wa kulinda wanyama kwenda ulipo mwili wa mama yake ambaye alikuwa
ameuawa katika mbuga moja ya kuhifadhi wanyama nchini India, kitendo
ambacho maafisa wa wanyama pori wanakilelezea kuwa si cha kawaida.
Askari wa wanyama pori ambaye alimwona mtoto wa
Simba akijificha vichakani, alimfuata na kugundua mwili wa Simba
aliyeuawa katika kilima jirani.
Mtoto huyo wa simba aliulinda mwili
wa mama yake hadi pale mlinzi wa wanyama pori aliporudi na maafisa wa
wanyama pori na polisi kuondoa mzoga huo.
Uchunguzi uliofanyiwa mwili wa simba huyo
ulibainisha kuwa alikufa katika mapigano na wanyama wengine huenda
aliuawa na kundi la nyati.
Naibu mhifadhi wa Misitu katika eneo la Gir,
Anshuman Sharma, amesema tabia ya simba huyo mtoto ni nadra kutokea na
ni cha aina yake, kitu ambacho hajawahi kushuhudia katika miaka yake
mingi ya kufuatilia tabia za simba.
Gir katika jimbo la Gujarat ni mahali
wanapopatikana kwa wingi simba wa Asia na kwa mujibu wa sense ya wanyama
iliyofanyika mwaka 2010, kuna simba 411 katika mbuga hiyo.
"Jumamosi mchana, nilikuwa nafanya doria katika
hifadhi ya Tulsi-Shyam nilipomwona mtoto wa simba akichificha katika
vichaka,"mlinzi wa msitu Rana Mori ameiambia BBC.
''Watoto wa Simba huambatana na mama zao''
Watoto wadogo wa simba nadra kuwakuta peke yao ,
kwa ujumla wanafuatana na mama zao na Bwana Mori anasema alianza
kumtafuta mama ya simba huyo mtoto.
"Nilimfuatilia mtoto wa simba ambaye aliniongoza
hadi kwenye mwili wa mama yake uliokuwa umelala katika kilima kidogo.
Simba huyo jike aliitwa Rupa [likiwa na maana ya Mzuri].Kwanza
alionekana kama aliyelala usingizi, lakini wakati hatikisiki,
nilimsukuma na fimbo yangu. Ndipo nilipogundua kwamba simba huyo jike
alikuwa amekufa," amesema.
Wakati Bwana Mori aliporejea na kundi la maafisa
kuondoa mzoga huo, walimkuta mtoto huyo wa simba akiwa amekaa kando ya
mwili wa mama yake.
Simba huyo jike ambaye alikuwa na umri wa miaka
kumi na moja , alivunjika mbavu na kupata majereha ya ndani na kufa
kutokana na kuvuja damu nyingi.
Mtaalam wa Simba Yadvendra Dev Jhala wa taasisi
ya Wanyama Pori ya India ameiambia BBC kuwa hajawahi kusikia tukio kama
hilo linalomhusu mtoto wa simba.
''Simba na walinzi wao''
Lakini amesema katika eneo la Gir hakuna mgogoro
kati ya simba na binadamu na "kwa ujumla Simba wanawafahamu vizuri
walinzi wao binafisi ".
Bwana Sharma anasema wanafahamika kwa tabia yao
ya maisha ya kijamii: "Si kama Mbwa, hawatoi kucha au kutikisa mikia,
lakini wanawatambua walinzi wanaowaona kila siku.."
Maafisa wa wanayama pori wanasema kwa ujumla
watoto wa simba ni wategemezi mno wa mama zao kwa ajili ya maisha yao
hadi wanapofikia umri wa miaka miwili na nusu hadi mitatu.
Mtoto huyo wa simba mwenye umri wa miezi 15, kwa sasa yuko chini ya uangalizi wa maafisa wa misitu.
"Mama yake, Rupa, alionekana kuwa mpweke na
aliwinda peke yake,Lakini kwa sasa simba huyo jike ametoweka,
tunatarajia mtoto huyo wa simba atajiunga na kundi lingine, au simba
mwingine jike huenda akaanza kumtunza," amesema Bwana Sharma.
0 maoni: