DAWA YA KUZUIA UKIMWI YAPATIKANA . SOMA HAPA KUJUA ZAIDI
WEKA TANGAZO
Watafiti
katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Temple, Marekani wamegundua
dawa ya kuangamiza Virusi Vya Ukimwi (VVU) ambayo ni ya uhakika zaidi
ukilinganisha na zilizowahi kupatikana katika tafiti za awali duniani.
Dawa yao inaweza kutumika kwa tiba ya wanaoishi na VVU na kinga kwa wale ambao bado hawajaambukizwa.
Mmoja
wa watafiti hao, Dk Kamel Khalili aliwaambia waandishi wa habari juzi
mjini Philadelphia, Marekani kuwa tofauti na utafiti mwingine, wao
wamegundua namna ya kukiondoa kirusi kilichoingia kwenye kinasaba (DNA)
ndani ya CD4 na kukitoa nje na hatimaye kukiua.
Alisema dawa hiyo inafanya kazi hiyo bila kuathiri seli za mwili wa binadamu.
Dk
Khalili alisema ugunduzi wao ni wa hali ya juu zaidi kwa sababu
teknolojia ya kutengeneza dawa hiyo ni tofauti na nyingine zilizokwisha
kugunduliwa ambazo hazina uwezo wa kupenya ndani ya seli za binadamu,
bali kuathiri tu VVU vilivyopo nje yake, ndani ya mfumo wa damu.
“Dawa
yetu inakivuta kirusi nje ya seli (CD4) bila kuiathiri seli yenyewe na
kukiua. Hivyo dawa hii itatumika kwa muda fulani na kuua virusi vyote
mwilini na hakuna haja ya kuitumia wakati wote kama ilivyo dawa ya
kufubaza VVU (ARV).”
ARV
huangamiza VVU vilivyopo kwenye damu na kuendelea kuviacha hai vile
ambavyo tayari vimeingia ndani ya CD4, hivyo kufanya virusi kuzuka upya
pindi mwathirika anapoacha kutumia dawa.
Mmoja
wa wataalamu katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu
Kituo cha Mbeya (NIMR-MMRC), Clifford Majani ameuelezea utafiti huo
kama mwanga mpya katika teknolojia ya kukabili VVU.
“Kama
imepatikana teknolojia ya kukiondoa kirusi ndani ya seli ni hatua nzuri
ya kukabili VVU. Hili lilionekana kuwa gumu mwanzoni,” alisema Majani.
Alisema
imekuwa vigumu kuua kirusi kikiwa ndani ya seli na hata baadhi ya
wanasayansi wamejaribu kutengeneza dawa itakayotambua seli
zilizoathirika ili ziuawe lakini hilo likawa gumu.
“Inaweza
ikapatikana dawa ya namna hiyo (inayoua seli zilizoathirika) lakini
ikawa inaathiri vitu vingine ndani ya mwili. Hilo halikubaliki. Kikubwa
katika ugunduzi huo ni dawa kuweza kukifuata kirusi kinakojificha na
kukiondoa, jambo ambalo dawa nyingi zimeshindwa zikiwamo ARV,” alisema.
Hata hivyo, Majani alisema changamoto ambayo inaweza kujitokeza katika majaribio ya dawa hiyo ni usalama wakati wa matumizi.
“Lazima
dawa hiyo ichunguzwe isije ikawa inaathiri viungo vingine pamoja na
utendaji wa mwili kwa ujumla. Maana hapo ndipo dawa nyingi
zinaposhindwa… Tusubiri tuone hii inaweza kuwa na matumaini zaidi,”
alisema Majani.
Mkutano wa Ukimwi
Ugunduzi
huo umekuja wakati wanasayansi, waunda sera na wadau wa mapambano ya
VVU wakiwa wanatoa kauli za kukata tamaa kwenye mkutano wa Ukimwi
unaomalizika kesho huko Melbourne, Australia.
Wanasayansi
kadhaa wanaotoka kwenye taasisi kubwa za utafiti za VVU wameweka wazi
kuwa tafiti nyingi zilizokuwa na matumaini zimeshindwa kufanya kazi kwa
asilimia 100 baada ya dawa zake kufanyiwa majaribio kwa sababu dawa zake
zinapotumika, vipimo huonyesha wamepona lakini baada ya muda VVU
hurejea upya.
“Kinachoonekana
ni kwamba virusi hivi hujificha sehemu fulani ya mwili ili visiathirike
na kusubiri mtu aache dawa ili virejee upya kushambulia CD4,” alisema
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya wa Magonjwa ya Kuambukiza na Kinga
ya Peter Doherty ya Australia, Profesa Sharon Lewin.
Dawa mpya inavyofanya kazi
Dk
Khalili alisema wametengeneza dawa yao kwa protini maalumu ambayo
inakata sehemu ya seli iliyoshambuliwa na kirusi cha Ukimwi na kukivuta
nje.
Baada
ya kukivuta, dawa huachana na seli hiyo na kuiacha ikijitibu yenyewe na
kupona kabisa kiasi cha kuendelea na kazi zake za kinga mwilini mwa
binadamu bila tatizo.
VVU kwa kawaida hushambulia seli kinga aina ya CD4 na kuzifanya kama kiwanda cha kuzalishia virusi vingine.
Kwa kawaida seli ikishaingiliwa na kirusi, huacha kazi yake ya kinga ya mwili na badala yake kuchukua jukumu la kutengeneza VVU.
“Dawa yetu inafanya kazi kwa haraka, kwa makini na bila kuathiri seli,” alijigamba Dk Khalili.
Alisema tayari imefanyiwa majaribio maabara na kuonekana inafanya kazi vizuri na sasa wamehamishia majaribio kwa wanyama.
Katika maabara, alisema dawa hiyo ilifanyiwa majaribio kwa damu ya binadamu na ikaonyesha kufanya kazi kwa asilimia 100.
Dk
Khalili anaamini kwamba majaribio hayo yatawachukua miaka michache...
“Lakini tunaamini ni mfumo ambao utaweza kufanya kazi vizuri kwa
binadamu.”
Alisema wanachofanya sasa ni kuangalia mfumo ambao utakuwa mzuri zaidi kwa ajili ya tiba ya binadamu.
Kwa
namna teknolojia ya dawa hiyo ilivyo, alisema wanaweza kuitumia kwa
ajili ya kuwatibu wale ambao tayari wameambukizwa na hata kuwakinga wale
ambao siyo waathirika.
Uzuri wa dawa hiyo, pia alisema inaweza kutumiwa na mtu ambaye anatumia ARV pasipo kuingiliana kiutendaji.
Ugunduzi
wao ulichapishwa kwenye Jarida la Taifa la Elimu ya Sayansi la National
Academy of Science la Marekani na kuonekana kuvuta hisia za wengi.
Hali ya Ukimwi duniani
Akizungumza
kwenye mkutano wa Melbourne, Profesa Lewin alisema tafiti za sasa
zinaonyesha kuwa karibu watu milioni 14 duniani wanaishi na VVU.
Alisema mamilioni ya watu hao wamekuwa wakisaidiwa kwa kutumia ARV, wakati huu ambao bado hakuna kinga wala tiba, inayoaminika.
Alisema
ingawa tafiti nyingi hazijaonyesha matumaini waliotarajia ya kupata
kinga na chanjo, bado juhudi zinaendelea ili kuhakikisha wanafikia
mahali HIV inakuwa haina nafasi katika mwili wa mwanadamu.
Alisema
pamoja na matokeo hasi ambayo yamejitokeza kwenye tafiti nyingi, bado
anaamini kwamba ipo siku chanjo na tiba vitapatikana.
Wanasayansi
waliohudhuria mkutano huo waliitaka dunia isiogope kutokana na
kushindwa kwa baadhi ya tafiti kama ilivyokuwa kwa mtoto wa Jimbo la
Mississippi, nchini Marekani ambaye alitangazwa amepona na baadaye
virusi vikaibuka upya.
WEKA TANGAZO
0 maoni: